HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Jumamosi, 2 Mei 2015

UNAJUA MEI DEI ILIANZANJE?

Leo Mei Mosi,wafanyakazi wamesherehekea siku ya Wafanyakazi, Mei Dei lakini unajua ilianzaje? Turudi nyuma mpaka tarehe 1 May 1886, Wafanya kazi 200,000 wa Marekani wakagoma wakidai kuwa wawe wanafanya kazi kwa masaa manane tu kwa siku. Siku hiyo, katika jiji la Chicago na miji mingine jirani wafanya kazi waligoma wakidai haki hiyo. Siku ya May 3 katika kiwanda kilichoitwa McCormick Reaper, mgomo ukageuka mapambano, na kesho yake mkutano wa amani ulioitwa baina ya waajiri na wafanyakazi ukabadilika kuwa mpambano mkubwa. Wanahistoria wanahadithia kuwa siku ya tarehe 4 May 1886 kiasi kama saa nne usiku mvua kubwa ilianza katika jiji la Chicago, waandamanaji waliokuwa wamekusanyika Haymarket Square, walianza taratibu kusambaratika, kabala ya hapo inasemekana walikuweko kama waandamanaji 3000 wakisikiliza hotuba za kulaani ukatiri wa polisi katika kudhibiti maandamano hayo, na huku madai ya siku ya kazi kuwa masaa manane yakiendelea, hivyo mvua ikawakimbiza wengi, hata Meya wa jiji aliyekuwa akitegemea fujo akawa kajua kuwa mambo yameisha na kuelekea kwake kulala. Msemaji wa mwisho alikuwa akimalizia mazungumzo yake ghafla polisi kama 180 wakaingia katika uwanja ule. Mkuu wa polisi akaamrisha watu watawanyike, ghafla bomu likatupwa kwenye kundi la polisi na kujeruhi polisi 67 na kuuwa saba. Hapohapo polisi wakaanza kutumia risasi za moto na kuuwa waandamanaji kadhaa na 200 wakajeruhiwa. Yaliyotokea Haymarket Square yakawa sehemu ya historia ya Marekani. Mwaka 1889 katika mkutano wa International Socialist Conference, ndipo ikatamkwa kuwa kwa kuweka kumbukumbu ya yaliyotokea Haymarket, May 1 iwe ni siku ya kimataifa ya mapumziko ya wafanyakazi. Kutokana na siasa za Marekani kupingana na usoshalist, mwaka 1958 Rais Eisenhower wa Marekani akatangaza kuwa May moja iwe Loyalty Day, siku ya kuonyesha uaminifu kwa nchi ya Marekani na kutambua Uhuru wa Wamarekani. Pamoja na kwamba siku hiyo ilianza Marekani , nchi hiyo husherehekea siku ya wafanyakazi mwezi September.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni