HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Jumatano, 26 Agosti 2015

MGOMBEA URAIS DR MAGUFULI KUFANYA ZIARA YA KAMPENI RUVUMA KUANZIA AUGUST 30
Picha kutoka maktaba

MGOMBEA Urais kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Dr. John Magufuli anatarajiwa kupokelewa na mamia ya wananchi wakiwemo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika kijiji cha Igawisenga wilayani Songea mkoa wa Ruvuma akitokea mkoa wa Njombe  tayari kuanza kampeni mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa  kamati ya maandilizi ya kampeni mkoani Ruvuma, Ramadhani Kayombo alisema kuwa Dr. Magufuli na msafara wake unatarajiwa kupokelewa Agosti 30 mwaka huu majira ya asubuhi huko katika kijiji cha Igawisenga.

Kayombo alieleza kuwa CCM imejipanga kikamilifu kwa kuhakikisha kuwa Dr. Magufuli, Wabunge na Madiwani wanafanyiwa kampeni za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni. Mgombea uraisi Dr. Magufuli anatarajia kufanya ziara za kampeni katika wilaya za Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru ambako atamaliza ziara Septemba 2, mwaka huu na kuendelea na ziara mkoani Mtwara.

Alisema kwa kuwa wananchi wengi wana imani na Chama Cha Mapinduzi na wanahitaji kumuona na kumsikiliza  hivyo amewataka wajitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni itakayofanyika wakati Dr. Magufuli akiwa mkoani humo, na pia amewaomba kuwa na mshikamano wa pamoja katika kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25  si vinginevyo.

 Habari kwa hisani ya  Jamvi la Habari Songea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni