HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Ijumaa, 4 Septemba 2015

MGOMBEA MWENZA BI SAMIA SULUHU AKIWA YOMBO BUZA MBELE KWA MBELE

MGOMBEA mwenza wa kiti cha urais Bi. Samia Suluhu amesema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetenga kiasi cha fedha kitakachotumika kama dhamana ili wajasiliamali mbalimbali wa jijini Dar es Salaam waweze kudhaminiwa kwenye mabenki na kupewa mikopo ili kuendeleza biashara zao.

Bi. Samia amesema hayo leo jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa kampeni Yombo Buza, Wilaya ya Temeke alipokuwa akiifafanua ilani ya Chama Cha Mapinduzi imepanga kuwafanyia nini Watanzania endapo watashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na kuunda Serikali ya CCM.

Mgombea huyo mwenza alisema Serikali ya CCM imepanga kujenga mazingira bora ya biashara kwa wajasiliamali ikiwa ni pamoja na kutenga fedha ambazo zitatumika kama dhamana katika mabenki ili kuwadhamini wajasiliamali hao kupewa mikopo ya kuendeleza na kuzikuza biashara zao.

Alisema Serikali pia itaweka utaratibu wa kuzilazimisha halmashauri nchini kuhakikisha asilimia 30 ya tenda zake zinafanywa na vikundi vya kijasiliamali vya vijana pamoja na wanawake ikiwa ni mkakati wa kuwainua vijana na akinamama kwenye biashara zao. Alisema halmashauri zimekuwa zikitoa tenda nyingi kwa makampuni ya kati hata zile ndogondogo hivyo utawekwa utaratibu tenda ndogo kwa sasa zifanye na vikundi hivyo.

Alisema ili kuongeza maeneo ya kufanyia biashara Serikali ya CCM itawekwa utaratibu mzuri ambao utakuwa ukifunga baadhi ya barabara na kuzitumia kama masoko ya muda kwa siku maalum kisha baadaye kufunguliwa na kuendelea na kazi zake. Kama hiyo aitoshi kodi ndogo ndogo zisizo na msingi zitafutwa ili kumuondolea bughudha ba kero wajasiliamali.

Aidha Bi. Suluhu aliongeza kuwa kwa Wilaya ya Temeke Serikali ya CCM imepanga kujenga masoko kadhaa likiwemo lile la Kijichi ambalo litachukua wafanyabiashara 580 kwa pamoja ili kuongeza fursa za biashara kwa akinamama na vijana, ardha ambayo tayari imeshatengwa na ilichobaki ni kuanza na ujenzi. Alibainisha kuwa Serikali itaanza kutenga asilimia 75 ya mapato ya halmashauri ili zirudi na kutumika kuzijenga barabara ndogondogo ikiwa ni jitihada za kuboresha miundombinu.

Aliongeza kuwa ili kuchochea ukuaji wa biashara kwa akinamama na vijana wajasiliamali Serikali itaanza kuwabana mgambo ambao wamekuwa wakiwabugudhi wafanyabiashara dogodogo ikiwa ni jitihada za kuondoa usumbufu kwao. 

Bi. Suluhu alisema miradi mingine ambayo Serikali inayoundwa na CCM imepanga kuisimamia kwa karibu ili kuboresha huduma hizo ni pamoja na uboreshaji huduma za afya, umeme kwa vijiji vyote vya Mkoa wa Dar es Salaam, uboreshaji huduma za maji safi na Salama, elimu pamoja na miundombinu ya barabara.

Mgombea huyo wa urais anaendelea na mikutano ya kampeni jijini Dar es Salaam baada ya jana kumaliza ziara ya kuinadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa wa Singida na Dodoma. 
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni