HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Alhamisi, 5 Novemba 2015

KARIBU DR MAGUFULI, WIZARA YA UTAMADUNI INATAKIWA KUANGALIWA UPYAA

Nakaa kwenye kiti nimetoka Uwanja wa Uhuru kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wetu mpya Dr John Pombe Magufuli. Dr Magufuli ameapishwa kuwa Rais wa nchi yetu kwa kipindi kijacho cha miaka mitano. Ilikuwa ndoto yangu kuwa yeye hatimae awe ndie kiongozi wa nchi hii na hakika blog hii ni ushahidi wa jitihada yangu ndogo katika kuchangia kufanikisha kwa ndoto hiyo. Leo Dr John Pombe Magufuli mbele ya umma wakiwemo viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali za Afrika ameapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Mungu ampe afya njema na maisha marefu.
Sikuwa nahangaika kupiga debe kupitia blog hii kwa Dr Magufuli awe Rais wetu kwa ushabiki tu, hapana, bali niliamini na ninaamini ataleta mabadiliko makubwa nchini kwetu katika Nyanja mbalimbali. Mimi ni msanii hakika nategemea mabadiliko makubwa katika tasnia inayonipa uhai wangu na wanangu, wasanii wenzangu, na rafiki zangu. Na nina uhakika kuwa Rais wetu mpya ataleta jibu.
Pamoja na kuoneka kuwa kuna maendeleo makubwa katika sanaa nchini Tanzania, ukweli ni kuwa hali ni sawa na kuwa na mpenzi mwenye sura nzuri inayotumia vipodozi vya gharama na hivyo kuonekana mrembo kabisa lakini kutojali sehemu nyingine za mwili. Hivyo ukionyesha picha yake ya passport utajua huyu ndie mrembo wa karne , ukiona picha ya mwili mzima ni mtu asiyeoga, kavaa nguo chakavu.
Hakika wengi watashanga kwa mtizamo wangu huu, na pengine hata kukumbusha kuwa siku hizi tuna wasanii vijana wazuri sana ambao wanajulikana hata nchi za nje,  na si kujulikana  tu bali hata kutwaa hata tuzo mbalimbali duniani sasa inakuwaje natoa mtizamo wa aina hii?
Ili kuweza kuelezea hili, ni vizuri kurudi nyuma miaka 20. Mara baada ya Rais wa awamu ya 3 kuingia madarakani, kulitokea mabadiliko makubwa katika sekta ya Utamaduni. Hakika wakati wa kutangaza orodha ya Wizara za serikali, Rais hakutaja Utamaduni. Wiki moja baada ya hapo Katibu Mtendaji wa BASATA alipoulizwa swali kuwa sekta ya Utamaduni iko Wizara ipi? Hata yeye hakuwa na jibu. Hakukuwa na tangazo rasmi lakini taratibu ilikuja onekana kuwa Utamaduni ilikuwa katika Wizara ya Elimu. Hapa lazima nikumbushe kuwa Utamaduni haijawahi kuwa Wizara ya kujitegemea, toka awali imekuwa ni Idara moja wapo katika Wizara na imeshakuwa kwenye Wizara zaidi ya 10 toka Uhuru. Utamaduni  ilipokuwa Wizara moja na Elimu ilikuwa ni tatizo kwani kipaumbele katika Wizara hii ilikuwa ni Elimu. Hivyo Utamaduni ilikuwa kama mtoto wa kufikia. Na katika kipindi hiki Maafisa Utamaduni Wilaya na Mkoa wakaondolewa  na hivyo kukawa hakuna kinacho waunganisha wasanii na wanautamaduni na Wizara iliyokuwa inahusika na Utamaduni. Katika Wilaya nyingine zilianza kuteua Maafisa Utamaduni ambao walikuwa chini ya Afisa elimu, ambaye nae alikuwa katika Wizara ya Tamisemi. Maafisa Utamaduni hawa walikuwa mara nyingi wakitumika kama watu wa kukusanya ushuru na kushughulikia Mwenge. Hadi leo kimsingi ndivyo hali ilivyo. Kwa msingi huu pamoja na kuwa kuna Wizara ya Utamaduni, lakini Maafisa Utamaduni hawako chini ya Wizara ya Utamaduni. Waziri wa Utamaduni hapangi bajeti yoyote kwa ajili ya Maafisa utamaduni kwani hawako katika Wizara yake na Waziri wa Tamisemi hashughuliki na Maafisa Utamaduni kwani hawako katika taratibu zake. Hivyo kwa miaka mingi sasa Utamaduni wa nchi hii umekuwa ukichukuliwa kiwepesi kabisa. Hili ni tatizo kubwa mno kuliko inavyoonekana. Watu wote duniani wana tamaduni zao. Kinachotofautisha taifa moja na jingine sio nguvu zao za kiuchumi, hilo hupimwa katika vipimo vya pato la nchi, uwezo wa kununua bidhaa au maendeleo yao ya kijamii. Hivyo ni vipimo tu vya kuonyesha uko ngazi gani katika dunia hii. Lakini katika swala la Utamaduni kila Taifa liko tofauti, hivyo kwa hilo wote tuko sawa hakuna aliyemzidi mwenzie. Katika Taifa kama letu lenye makabila zaidi ya 120, pia kila kabila linatambulika kuwa sawa na jingine kutokana na tamaduni za kabila husika. Uwingi huu wa tamaduni ndogo (sub-cultures) ni baraka kubwa kwa Taifa letu, baraka ambazo ilitakiwa kuwafunza wananchi wa Taifa hili kuzilea na kuzithamini na kuzikuza. Tusikosee na kuanza kujilinganisha na kujipima kulingana na tamaduni nyingine; kuwa na tamaduni tofauti na nyingine ndio umuhimu mkubwa wa utamaduni wetu. Kama Taifa ni muhimu kujali Utamaduni wetu, urithi wetu wa kiutamaduni. Kutokana na pengo la mkono wa serikali katika utamaduni, wafanyabiashara wamechukua nafasi yao katika kuendeleza vijisehemu tu vya sanaa ambavyo vina leta mapato ya haraka haraka, na mara nyingine hata kutumia fehda kuhakikisha tamaduni wasizozipenda zinafutika. Takwimu za BASATA za mwaka 2006 zilikisia kuwa katika kila kaya tano kuna msanii, ilionekana kulikuwa na wasanii zaidi ya milioni 6 hapa nchini. Hili ni kundi kubwa la wananchi ambalo kuliacha halina mwongozo ni kupoteza mambo mengi muhimu ya Taifa hili. Bahati mbaya sana maana ya wasanii siku hizi huchukuliwa tu kuwa ni wale wanamuziki au wacheza filamu maarufu. Lakini kwa takwimu hizo hapo juu ni wazi Tanzania ina mamilioni ya wasanii, kila kijiji nchini, wasusi, wafinyanzi, wachoraji wachongaji, wanamuziki, waigizaji na aina nyingi mno za wasanii. Wengi wa hawa wasanii, usanii wao ndio ajira zao. Kwa mfumo ambao umekuweko katika miaka mingi wananchi hawa wamekuwa wametoswa pembeni bila kuwa na mwongozo wala taratibu za kuboresha sanaa yao. Kutokuweko na mfumo mzuri wa kiserikali katika sekta ya Utamaduni sio tu imakuwa hasara kwa Utamaduni na wasanii, bali pia kwa pato la serikali kwani ripoti ya WIPO ya mwaka 2007 ilionyesha kuwa pato la sekta ya ubunifu ni kubwa kuliko usafirishaji, gesi, madini na kadhalika.
Ukosefu wa taratibu ulipelekea hata wasanii kuona kuwa jibu la matatizo yao ni kukimbilia Ikulu, jambo ambalo si rahisi kwa kila msanii kulifikia.
Hivyo basi jambo kubwa kama msanii ninalotegemea katika awamu hii ni kupata Wizara itakayokuwa ina mtiririko utakaoweza kuwatumikia wabunifu na wasanii kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa, hili litaweza kufukua vipaji kutoka chini, kuongeza ajira kwa wabunifu kutoka ngazi ya chini, na kuongeza pato la Taifa kutokana na kazi za ubunifu Hilo pia litafundisha Uzalendo na Utaifa kwa wananchi wote, na hivyo kupata nembo ya Utanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni