HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Ijumaa, 20 Novemba 2015

MSANII NILIVYOIPOKEA HOTUBA YA RAIS KUZINDUA BUNGE LA 11


FB_IMG_1438963514104-1
KWA MUDA MREFU wasanii wazalendo wengi tumekuwa tunakereketwa na mengi yaliyokuwa yanafanyika katika nchi hii dhidi ya wasanii na wabunifu. Watu wote duniani wana tamaduni zao. Kinachotofautisha taifa moja na jingine sio nguvu zao za kiuchumi, hilo hupimwa katika vipimo vya pato la nchi, uwezo wa kununua bidhaa au maendeleo yao ya kijamii. Hivyo ni vipimo tu vya kuonyesha uko ngazi gani katika dunia hii. Lakini katika swala la Utamaduni kila Taifa liko tofauti, hivyo kwa hilo wote tuko sawa, kwani ni kwa kupitia kigezo cha Utamaduni ndipo ambapo nasi tunasimama bila aibu kushindania na Taifa lolote duniani. Katika Taifa kama letu lenye makabila zaidi ya 120, pia kila kabila linatambulika kuwa sawa na jingine kutokana na tamaduni za kabila husika. Uwingi huu wa tamaduni ndogo (subculture) ni baraka kubwa kwa Taifa letu, baraka ambazo tunatakiwa tujifunze namna ya kuzilea na kuzithamini na kuzikuza, ili tuweze kuendelea kusimama kifua mbele tukiwa kama Taifa. Tusikosee na kuanza kujilinganisha na tamaduni nyingine, kwani kwa kuwa na tamaduni tofauti na nyingine ndio thamani kubwa ya utamaduni wetu. Kama Taifa ni muhimu kujali Utamaduni wetu, urithi wetu wa kiutamaduni, na wakati huohuo kuangalia wakati ujao na kujipanga kulea na kuendeleza Utamaduni wetu katika ulimwengu huu ambao sasa umekuwa kama kijiji. Kwa mtazamo huo basi wasanii ambao tumekuwa tukijua kazi nyingi na nzuri za sanaa zinatengenezwa Tanzania ZINGETUMIWA ipasavyo na Watanzania, zingeleta hali ya kujitambua , kujivunia Utanzania, na kuhakikisha ajira kwa Watanzania. Kuna mambo yalikuwa yana umiza roho sana , kwa mfano WIZARA katika serikali ya Tanzania kuagiza kundi la Makirikiri kutoka Botswana kwa ajili ya sherehe ya Wizara hiyo. Je, ni kweli hakuna vikundi Tanzania vinavyoweza kucheza ngoma mpaka hata ngoma za kiasili kuagiza Botswana? Balozi zetu zingetumia sanaa kutoka Tanzania, hakika zingekuwa na sura tofauti yenye utambulisha wa Tanzania, uamuzi huo ungewezesha wasanii wa Tanzania kupata kipato, ungesaidia wasanii kutambulika katika nchi ambazo kazi hizo zipo na kuchangia katika kukaribisha watalii nchini Tanzania. Uamuzi wa kutumia samani za Tanzania utahakikisha mafundi seremala wa Kitanzania wanapata ajira, kipato na wao kuchangia pato la nchi. Kutambuliwa kwa wasanii kama ni kundi maalumu katika hotuba ya Rais, kuna onyesha siku mpya katika kundi hili. Katika ripoti ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikisiwa kuwa ni kiasi cha milioni sita. Kwa kuwa ni miaka tisa sasa imepita toka wakati wa ripoti hiyo kuna kila sababu ya kuamini kuwa kundi hilo limekuwa kubwa zaidi. Mara nyingi sana watu wengi hudhani wasanii ni wanamuziki na waigizaji tu, hiyo si kweli karibu kila nyumba nchini ina msanii, wasusi, wafinyanzi, wachoraji, waimbaji, na wasanii wengine wa aina mbalimbali ambao wengine maisha yao na familia zao hutegemea kazi zao za kisanii, kwa ukweli huu kila kijiji kina wasanii na hili ni kundi kubwa la watu. Ukitaja wafugaji, ndani yake kuna wasanii, ndani ya wakulima wamo wasanii, na kila kundi lina wasanii, na bada ya hapo kuna kundi kubwa la wanaohudumia wasanii au wanotegemea wasanii hawa au kazi zao ili waishi,watu kama wafanyakazi wa vyombo vya utangazaji, wafanya kazi katika biashara ya matangazo, wasambazaji, wafanya biashara ndogondogo, (machinga) na wengine wengi waliomo katika mnyororo wa biashara hii ikiwemo, maproducer, mameneja, mafundi mitambo, watayarishaji wa maonyesho na kadhalika. Hivyo sanaa si utamaduni tu bali ni kazi yenye nafasi kubwa ya ajira na mapato makubwa. Ripoti ya WIPO ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa kazi zitokanazo na Hakimiliki huingiza mapato zaidi katika uchumi wa Taifa kuliko MADINI, jambo ambalo ni wazi wengi wanaosikia kwa mara ya kwanza hushangaa na hata kubisha, na hasa kwa kuwa kelele za mapato ya Madini ni kubwa sana katika jamii wakati hakuna anaelalamika kuhusu mapato kutokana na raslimali ya nchi inayoitwa sanaa. Ripoti hiyo ya WIPO pia ilionyesha kuwa sekta ya Hakimiliki inaajiri watu wengi zaidi kuliko, sekta za Madini, gesi, maji, Ustawi wa Jamii, Afya, Usafirishaji. Hivyo ni sekta ambayo ina umuhimu sana katika uchumi wa Taifa ikiwa italindwa inavyostahili. Hotuba ya Rais imeleta matumaini mapya katika tasnia ya Sanaa. 
 John Kitime

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni