HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Jumatatu, 8 Agosti 2016

STAMICO YAWATANGAZIA NEEMA WACHIMBAJI WA MADINI TANZANIA


Katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika na kazi zao na kuepuka kuondolewa na wachimbaji wakubwa wameshauriwa kuchukua leseni ndogo za awali za uchimbaji.
STAMICO Nane nane 2016 -1
Kaimu Mkurugenzi wa utafiti na Uchimbaji wa Shirika la Madini (STAMICO) Alex Rutagwelela (Katikati) akiongea na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa maonyesho ya Nane nane Viwanya vya Ngongo - Lindi.

Wito huo kwa wachimbaji umetolewa na kaimu mkurugenzi wa utafiti na uchimbaji wa shirika la madini (STAMICO) Alex Rutagwelela alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya ngongo Manispaa ya Lindi yanapofanyika maonyesho ya nane nane kitaifa.

Rutagwelela alisema wachimbaji wadogo wanatakiwa kuwa na leseni za awali zitakazowafanya wawe na haki kwenye maeneo wanayochimba. hivyo kuwa na uhakika wa kuto ondolewa bila taratibu na wachimbaji wakubwa kwenye maeneo wanayochimba.
STAMICO Nane nane 2016 -2
Wananchi wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Maafisa wa STAMICO walipotembelea Banda lao katika Maonyesho ya Nane nane yanayoendelea Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo.

Aliwahakikishia wanahabari na wananchi shirika hilo linania ya kuwainua wachimbaji wadogo kwa kufanyia tathimini maeneo wanayochimba ili waweze kujua kiasi cha madini na mashapo yaliyopo katika maeneo hayo.

Alisema wachimbaji wanaweza kupata fursa ya mafunzo ili waweze kupata ujuzi wa kuyafahamu mambo ya kijiolojia, vilevile watakuwa na uwezo wa kupata mikopo. 

Hata hivyo alitahadharisha kwamba wanaweza kunufaika na fursa hizo ni wachimbaji wenye leseni.
"Wachimbaji wenye leseni nilazima wainuliwe, wengi wao hawana mitaji wanachimba kipindi cha masika kwenye makorongo na kiasi wanachopata ni kidogo sana, kwamfano wilaya ya Ruangwa na mkoa huu unamadini ya aina nyingi na mengi wakiwezeshwa watanufaika," alisema Rutagwelela.
STAMICO Nane nane 2016 -3
Akibainisha wachimbaji wadogo wanachimba kwa kubahatisha, hivyo shirika hilo lipotayari kuwasaidia kufanya tathimini na kuwaonesha kiasi cha mashapo yaliyopo katika maeneo wanayochimba. 

Huku akitoa wito wawe tayari kwa uchangiaji kiasi kidogo cha fedha ambacho ni rafiki kwa wachimbaji wadogo kwa ajili ya gharama ya uendeshaji mitambo wakati wa kuchoronga, ikiwamo mafuta.

Akiongeza kusema STAMICO kwa niaba ya serikali imejipanga kuwasaidia kufikia malengo yao ya kiuchumi na kimaendeleo.

Ijumaa, 5 Agosti 2016

DIWANI WA CHADEMA ASWEKWA NDANI KWA KUKIUKA MAAZIMIO YA BARAZA LA MADIWANI WILANI IKUNGI


Na Mathias Canal, Singida
Jeshi la polisi Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida limemtia nguvuni Diwani wa Kata ya Iseke kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Emmanuely Njingu kwa kosa la kukwamisha shughuli za serikali kwa kuzuia watendaji wa serikali kufanya kazi yao ikiwemo ukusanyaji wa mapato.

Njingu ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya fedha awali kabla ya kuwekwa nguvuni na jeshi la polisi alivuliwa ujumbe wa kamati hiyo kutokana na kukiuka taratibu na makubaliano ya baraza la madiwani jambo ambalo limepelekea kuhamishiwa katika kamati nyingine.

Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa diwani huyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni Diwani wa Kata ya Irisia Ally Juma Mwanga amesema kuwa Diwani huyo amekamatwa kwa mujibu wa sheria hivyo yeye kama mwenyekiti hawezi kuingilia taratibu, sheria,na kanuni za serikali.

Mwanga amesema kuwa tarehe 19 mwezi Julai moja ya maazimio ya kamati ya fedha na vikao vya baraza ilikuwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri lakini diwani huyo amekiuka makubaliano hayo kwa kung’oa mageti ya vizuizi vya barabarani kwa ajili ya ukaguzi wa mazao jambo ambalo limepelekea kuzorota kwa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.

Ameongeza kuwa Mjumbe yeyote anayekiuka maazimio wanayokubaliana na kutoa siri za kamati adhabu yake kisheriani kupoteza sifa ya kuwa mjumbe wa kamati husika.

Amesema diwani huyo ameondoshwa katika nafasi hiyo baada ya maridhiano ya kamati hiyo na kukubaliana kumuhamishia katika kamati nyingine ya huduma za uchumi.

“Jambo mkishakubaliana kisheria tena kwenye vikao vya kisheria maana yake linakuwa ni sheria hivyo kwa kiongozi yeyote akikiuka taratibu za kisheria zinachukua mkondo wake, kanuni za Halmashauri ni za watu wote hazichagui upande mmoja” Alisema Mwanga

Hapo jana Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu alihutubia Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ikiwa ni mara yake ya mwanzo kabisa tangu alipochaguliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambapo pamoja na kuzungumzia kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa maabara, afya duni na miundombinu pia alizungumzia kuhusu ukusanyaji hafifu wa mapato jambo ambalo linairudisha nyuma Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Bajeti ya Wilaya ya Ikungi kwa Mwaka 2013/2014 ilikuwa na Shilingi 509,701,044 namakusanyoyakeyakawa ni 338,325,000 ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kuwa na upungufu wa shilingi 171,376,044.

Mwaka 2014/2015 ilipangwa bajeti ya shilingi 631,455,000 lakini makusanyo yake yakawa ni shilingi 457,555,172 ambapo mwaka ulimalizika kwa kukusanya 173,899,828.

Mwaka wa bajeti 2015/2016 bajeti ya Halmashauri iliyopangwa ilikuwa ni shilingi 1,127,030,000 makusanyo yalikuwa ni 679,283,000 ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kwa kuwa na upungufu wa shilingi 450,747,000 hivyo kwa miaka mitatu Halmashauri hiyo imeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji.

Mwanga amesema kuwa Kutofikiwa malengo hayo kumesababishwa na kutopewa ushirikiano watendaji katika ukusanyaji wa mapato hii ikiwa ni kufuatia kauli za mazuio zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.

Hata hivyo ametoa Mwito kwa viongozi wa serikali, wanasiasa, taasisi za dini na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kufikia malengo ya kuifanya Ikungi kukua kiuchumi .