HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Jumamosi, 8 Aprili 2017

URUSI YATOA ONYO WAKATI MAREKANI YATISHIA KIPIGO ZAIDI KWA SYRIA


Urusi na Marekani wametupiana maneno makali wakati wa kikao cha dharura cha UN Security Council kilichoitishwa na Urusi baada ya jeshi la Marekani kurusha makombora kwenye kituo cha jeshi la ndege za Syria.
Jeshi la Syria lilitoa taarifa kuwa watu 6 walifariki katika shambulio hilo ambalo Marekani ilitupa makombora karibu 60 ya aina ya Tomahawk ili kukiharibu kituo cha ndege cha Shayrat, ambako Marekani inaamini ndiko zilipotoka ndege zilizotupa makombora ya gesi ya sumu yaliyouwa wananchi mapema wiki hii.
Vladimir Safronkov, ambaye ni Balozi msaidizi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, aliilani Marekani kwa nguvu kutokana na kitendo hicho alichokiita ni uvunjaji wa sheria za kimataifa, Balozi huyo alisema kitendo hicho kinatishia amani ya dunia kwa ujumla.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani katika UN, Bi. Nikki Haley alisema Marekani ilikuwa na haki kabisa kutumia nguvu za kijeshi na iko tayari kwa kufanya mengine zaidi.
Taasisi ya Syrian Observatory for Human Rights iliyoko Uingereza inadai kuwa si chini ya watu 88 wakiwemo watoto 29, waliuwawa kwa gesi ya sumu huko Khan Sheikhoun katika jimbo la Idlib. Marekani inadai sumu hiyo ilidondoshwa na majeshi ya Syria.
 Pamoja na Marekani kudai kuwa makombora yake 58 kati ya 59 yaliyorushwa yalipiga kilicholengwa na kutia hasara kubwa kwa uwanja wa ndege na vifaa vya  jeshi la Syria, lakini picha za satellite zinaonyesha kuwa uwanja huo haukupata hasara kubwa sana na kwa upande wake Syria inadai ni makombora 23 tu yaliyoweza kutia hasara. Masaa 24 baada ya hapo uwanja huo ulianza kutumika tena.
Serikali ya Syrian, imejitetea kuwa gesi hiyo ilitokana na ndege zake kupiga ghala la mabomu ya gesi hiyo yaliyokuwa yakimilikiwa na waasi. Nchi nyingi za Magharibi zinapinga utetezi huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni