HATUPIMI BANDO

HATUPIMI BANDO

Jumatatu, 10 Julai 2017

ZI WAPI SEHEMU ZA UMMA ZA KUCHEZA WATOTO

Siku chache zimepita toka sikukuu  kubwa ya Idd imepita, na tumeona jambo moja limerudia tena ambalo hutokea kila ijapo sikukuu kubwa yenye shamra shamra nyingi. Mamlaka hutamka kuwa ‘Disco Toto” zimepigwa marufuku. Hii amri haijaanza kutolewa mwaka huu, hakika ilianza kutolewa baada ya mikasa mibaya kutokea kutokana na watoto kupata madhara makubwa kutokana na kujazana sana kwenye ‘Disco Toto’.  Disco Toto ni jina jipya lakini dhana ya watoto kufurahia sikukuu kwa kucheza muziki ni jambo ambalo lililomo kwenye utamaduni wetu, hakika wanaotoa amri ya kupiga marufuku Toto Disco waliwahi kuwa watoto na wanakumbuka furaha ya siku ya sikukuu, kuvalishwa nguo mpya kutoka kwenda kutembea, kwa wale wa Dar es Salaam wanakumbuka uwanja wa Mnazi Mmoja ulivyokuwa unachangamka siku kama hii, upande ule wenye jukwaa, ambalo kwa sababu wazijuazo viongozi wa sasa wa  Jiji hili jukwaa hilo halitumiki tena, wakubwa hawa kama walikuwa wakazi wa Dar es Salaam wanakumbuka enzi za utoto wao jinsi  uwanja wa Kidongo Chekundu ulivyokuwa ukichangamka kwa aina mbalimbali za starehe zikiwemo muziki, michezo mbalimbali, vyakula na vinywaji, uwanja huu umebadilishwa matumizi.  Kwa wazee wale waliokulia Dar es Salaam wanakumbuka enzi ukumbi wa Arnatouglo ulivyokuwa eneo muhimu la watoto kufurahi na kucheza muziki wa bugi, muziki uliokuwa ukipigwa mchana mwisho saa kumi na mbili, na hata  wanamuziki wenyewe pia wengi wakiwa watoto, jumba hilo limebadilishwa matumizi . Enzi za utoto wao wakubwa hawa, majumba ya sinema yalikuwa yakijaa siku za sikukuu, jijini Dar es Salaa kulikuwa na majumba maarufu ya Cameo, Avalon, Chox, Drive in, Empire na Empress, majumba yote haya yamebadilishwa  matumizi. Na hivyo ndivyo ilivyo katika miji yote, kwa mimi niliyekulia Iringa, ambaye wakati nikiwa mtoto siku za sikukuu nilienda kucheza dansi la mchana katika ukumbi wa Community Center pale Kitanzini, dansi ambalo liliisha saa kumi na mbili na meneja wa ukumbi alihakikisha hata kwa kuzima umeme kuwa dansi linaisha saa kumi na mbili, sehemu hii ilikuwa ukumbi wa wazi wenye nafasi na mzunguko mzuri wa hewa, ukumbi  huu nao  umebadilishwa matumizi. Iringa ilikuwa na kumbi mbili za sinema, Highland na Paradise au Tivoli, ambazo siku za sikuu watoto tulijazana kuangalia sinema kwa ratiba maalumu ya sikukuu, zilizoanza kuonyesha sinema  saa nne asubuhi, na watoto wasiosindikizwa na wazazi mwisho kuingia sinema ilikuwa saa kumi na mbili jioni, kumbi hizi zote zimebadilishwa matumizi. Na hadithi hiyo ndivyo ilivyo kila kona katika nchi hii. Sasa hali hii inasikitisha, watu wameongezeka sana, hivyo watoto ni wengi zaidi, sehemu ambazo watoto walikuwa wakiweza kupata nafasi japo siku za sikukuu kufurahi, zimenyang’anywa na kugeuzwa matumizi ya wakubwa na mamlaka, na hakuna kitu mbadala kilichotengenezwa kwa ajili ya watoto.  Wafanya biashara ndio wameachiwa kazi ya kutengeneza mazingira ya kuhakikisha watoto wetu wanafurahi na kucheza siku za sikukuu, asilimia kubwa ya sehemu za burudani zinazoendeshwa na wafanyabiashara zinaongozwa na taratibu za kupata faida hivyo huko ulevi, matusi, maadili maovu sio tatizo, na hizo ndizo sehemu ambazo tumewaachia watoto wetu baada ya kuwanyanganya sehemu salama. Swala la kupiga marufuku ni swala rahisi sana, lakini kinachotakiwa na wakuu hawa ni kujenga mazingira ya watoto kufurahi salama, kwani amri ya kupiga marufuku haiongezi chochote chenye tija, na kama hakuna jambo la ziada litakalofanyika, kila sikukuu tutasikia tena na tena amri ya kuwa ‘Disco toto’ limepigwa marufuku. Sitaacha kusema kuwa watoto na vijana hawatendewi haki. Sehemu zao salama za kukusanyika zimetoweka na hakuonekani mpango wowote wa kuwatengenezea mazingira ya kukua katika malezi mema. Mitaa imejazana watoto wakitaka kucheza lazima wacheze barabarani au vichochoroni au waende umbali mkubwa kutoka kwao ili kupata nafasi za wazi za kucheza kwa furaha, hakika kwa Taifa ambalo linadai linawatetezi wa haki za binadamu ububu katika hili unashangaza sana. Au haki za binadamu zinakuja inapoongelewa haki za kisiasa tu? Watoto na vijana hawana haki ya kutengewa mazingira salama ya kufurahi? Wazazi tuamke kudai haki hizi za watoto wetu, au nchi hii ni ya wakubwa tu? 
Article 31 of the U.N. Convention on the Rights of the Child (adopted by the General Assembly of the United Nations, November 20, 1989), which states that the child has a right to leisure, play, and participation in cultural and artistic activities. Kwa Kiswahili chepesi ibara hii ya tamko la Haki za Mtoto la Umoja wa Mataifa linasema mtoto ana haki ya  kustarehe, kucheza na kushiriki katika shughuli za kiutamaduni na kisanii.Au na hili nalo mpaka tusaidiwe na wafadhili?

 Angalia ramani zinazotengenezwa za miji mipya, Je maeneo ya watoto yapo? Au zote zimejaa sehemu za majumba ya kulala na shopping Malls. Kila wanapoishi wakubwa watoto watakuwepo, tuwe tunawajumuisha katika mipango yetu, na sio kukumbuka kupiga marufuku wasifurahie utoto wao.Bahati mbaya hata kwenye ngazi ya familia, wazazi wakiona kuna kanafasi mbele au nyuma ya nyumba yao, hata kama wana watoto sita wanachowaza kwanza ni kukodisha eneo hilo kupata fedha, wazo kuwa watoto wake mwenyewe wanahitaji eneo la kujidai hutoweka mbele ya ndoto ya fedha za harakaharaka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni